Mit. 25:6-19 Swahili Union Version (SUV)

6. Usijitukuze mbele ya uso wa mfalme;Wala usisimame mahali pa watu wakuu;

7. Kwa maana ni heri kuambiwa, Njoo huku mbele;Kuliko kuwekwa nyuma machoni pa mkuu.Yale uliyoyaona kwa macho,

8. Usitoke nje kwa haraka ili kuyashindania;Usije ukakosa kujua la kutenda hatimaye,Mwenzako atakapokuwa amekuaibisha.

9. Ujitetee na mwenzako peke yake;Bali usiifunue siri ya mtu mwingine;

10. Yeye asikiaye asije akakutukana;Na aibu yako isiondoke.

11. Neno linenwalo wakati wa kufaa,Ni kama machungwa katika vyano vya fedha.

12. Kipuli cha dhahabu, na pambo la dhahabu safi;Ndivyo alivyo mwonyaji mwenye hekima kwa sikio lisikialo.

13. Kama baridi ya theluji wakati wa mavuno;Ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwao wamtumao;Kwa maana huwaburudisha bwana zake nafsi zao.

14. Kama mawingu na upepo pasipo mvua;Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo.

15. Kwa uvumilivu mwingi mkuu husadikishwa;Na ulimi laini huvunja mfupa.

16. Je! Umeona asali? Kula kadiri ya kukutosha;Usije ukashiba na kuitapika.

17. Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi;Asije akakukinai na kukuchukia.

18. Mtu amshuhudiaye jirani yake uongoNi nyundo, na upanga, na mshale mkali.

19. Kumtumaini asiye mwaminifu wakati wa taabuNi kama jino lililovunjika, au mguu ulioteguka.

Mit. 25