Mit. 20:10-27 Swahili Union Version (SUV)

10. Vipimo mbalimbali, na pishi mbalimbali,Vyote viwili ni chukizo kwa BWANA.

11. Hata mtoto hujijulisha kwa matendo yake;Kwamba kazi yake ni safi, kwamba ni adili.

12. Sikio lisikialo, na jicho lionalo,BWANA ndiye aliyeyafanya yote mawili.

13. Usipende usingizi usije ukawa maskini;Fumbua macho yako nawe utashiba chakula.

14. Haifai kitu, haifai kitu, asema mnunuzi;Lakini akiisha kwenda zake hujisifu.

15. Dhahabu iko, na marijani tele;Lakini midomo ya maarifa ni kito cha thamani.

16. Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni;Mtoze rehani aliye mdhamini wa wageni.

17. Chakula cha uongo ni kitamu kwa mtu;Lakini halafu kinywa chake kitajaa changarawe.

18. Kila kusudi huthibitika kwa kushauriana;Na kwa shauri la akili fanya vita.

19. Mwenye kitango akisingizia hufunua siri;Basi, usishirikiane naye afunuaye midomo yake sana.

20. Amlaaniye babaye au mamaye,Taa yake itazimika katika giza kuu.

21. Urithi uliopatikana mwanzo kwa haraka,Mwisho wake, lakini, hautabarikiwa.

22. Usiseme, Mimi nitalipa mabaya;Mngojee BWANA, naye atakuokoa.

23. Vipimo mbalimbali ni chukizo kwa BWANA;Tena mizani ya hila si njema.

24. Mwenendo wa mtu watoka kwa BWANA;Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake?

25. Ni mtego, mtu aseme kwa haraka, Kitu hiki ni wakfu;Na baada ya kuweka nadhiri kuuliza-uliza habari.

26. Mfalme mwenye hekima huwapepeta wasio haki;Naye hulipitisha gurudumo la kupuria juu yao.

27. Pumzi ya mwanadamu ni taa ya BWANA;Hupeleleza yote yaliyomo ndani yake.

Mit. 20