Mit. 15:5-23 Swahili Union Version (SUV)

5. Mpumbavu hudharau kurudiwa na babaye;Bali yeye aangaliaye maonyo hupata busara.

6. Katika nyumba ya mwenye haki mna akiba nyingi;Bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tu.

7. Midomo ya mwenye haki hueneza maarifa;Bali moyo wa mpumbavu haufanyi hivyo.

8. Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA;Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake.

9. Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA;Bali humpenda mtu afuatiaye wema.

10. Adhabu kali ina yeye aiachaye njia;Naye achukiaye kukemewa atakufa.

11. Kuzimu na Uharibifu vi wazi mbele za BWANA;Si zaidi basi, mioyo ya wanadamu?

12. Mwenye mzaha hapendi kukaripiwa;Wala yeye hawaendei wenye hekima.

13. Moyo wa furaha huchangamsha uso;Bali kwa huzuni ya moyo roho hupondeka.

14. Moyo wa mwenye ufahamu hutafuta maarifa;Bali kinywa cha wapumbavu hula upumbavu.

15. Siku zote za mtu ateswaye ni mbaya;Bali ukunjufu wa moyo ni karamu ya daima.

16. Kuwa na mali chache pamoja na kumcha BWANA;Ni bora kuliko mali nyingi pamoja na taabu.

17. Chakula cha mboga penye mapendano;Ni bora kuliko ng’ombe aliyenona pamoja na kuchukiana.

18. Mtu wa hasira huchochea ugomvi;Bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano.

19. Njia ya mtu mvivu ni kama boma la miiba;Bali mapito yao wenye unyofu hufanyika njia kuu.

20. Mwana mwenye hekima humfurahisha babaye;Bali mpumbavu humdharau mamaye.

21. Upumbavu ni furaha kwake aliyepungukiwa na akili;Bali mwenye ufahamu huunyosha mwenendo wake.

22. Pasipo mashauri makusudi hubatilika;Bali kwa wingi wa washauri huthibithika.

23. Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake;Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!

Mit. 15