13. Ndipo nilipoona ya kuwa kweli hekima hupita upumbavu, kwa kadiri nuru ipitavyo giza;
14. macho yake mwenye hekima yamo kichwani mwake, lakini mpumbavu huenda gizani; ila hata hivyo nikatambua ya kwamba ni tukio moja la mwisho liwapatalo wote sawasawa.
15. Nikasema moyoni mwangu, Kama limpatavyo mpumbavu, ndivyo litakavyonipata mimi nami; basi, kwa nini nikawa na hekima zaidi? Nikasema moyoni mwangu ya kuwa hayo nayo ni ubatili.
16. Maana hakuna kumbukumbu la milele la mwenye hekima, wala la mpumbavu; kwa sababu siku zijazo wote pia watakuwa wamekwisha kusahauliwa. Na mwenye hekima, jinsi gani anavyokufa sawasawa na mpumbavu!
17. Basi, nikauchukia uhai; kwa sababu kazi inayotendeka chini ya jua ilikuwa mbaya kwangu; yaani, mambo yote ni ubatili na kujilisha upepo.
18. Nami nikaichukia kazi yangu yote niliyojishughulisha nayo chini ya jua; maana sina budi kumwachia yeye atakayenifuata.