Mdo 10:22-41 Swahili Union Version (SUV)

22. Wakasema, Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako.

23. Akawakaribisha wawe wageni wake.Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye.

24. Siku ya pili yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwangojea, hali amekusanya jamaa zake na rafiki zake.

25. Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguu, akamsujudia.

26. Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu.

27. Na katika kusema naye akaingia ndani, akaona watu wengi wamekusanyika.

28. Akawaambia, Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine wala kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote mchafu wala najisi.

29. Kwa sababu hiyo nalikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani mliloniitia?

30. Kornelio akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa ii hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, mwenye nguo zing’arazo,

31. akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu.

32. Basi, tuma watu kwenda Yafa, ukamwite Simoni aitwaye Petro, anakaa katika nyumba ya Simoni, mtengenezaji wa ngozi, karibu na pwani; naye akija atasema nawe.

33. Mara nikatuma watu kwako, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tupo hapa mbele za Mungu, tupate kuyasikiliza maneno yote uliyoamriwa na Bwana.

34. Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;

35. bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.

36. Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote),

37. jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliouhubiri Yohana;

38. habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.

39. Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini.

40. Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika,

41. si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.

Mdo 10