Law. 9:8-19 Swahili Union Version (SUV)

8. Basi Haruni akakaribia madhabahuni, akamchinja huyo mwana-ng’ombe wa sadaka ya dhambi, aliyekuwa kwa ajili ya nafsi yake.

9. Kisha wana wa Haruni wakamsongezea Haruni ile damu; naye akatia kidole chake katika damu, na kuitia katika pembe za madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu;

10. lakini mafuta, na figo, na kitambi kilichotoka katika ini ya hiyo sadaka ya dhambi, akaviteketeza juu ya madhabahu, kama BWANA alivyomwagiza Musa.

11. Na nyama, na ngozi akazichoma moto nje ya marago.

12. Naye akaichinja sadaka ya kuteketezwa; na wanawe Haruni wakamsongezea ile damu, naye akainyunyiza katika madhabahu pande zote.

13. Nao wakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, na kichwa; naye akaviteketeza juu ya madhabahu.

14. Kisha akaosha matumbo, na miguu na kuiteketeza juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa madhabahuni.

15. Kisha akaisongeza dhabihu ya watu, akamtwaa mbuzi wa sadaka ya dhambi aliyekuwa kwa hao watu, na kumchinja, na kumtoa kwa ajili ya dhambi kama yule wa kwanza.

16. Kisha akaisongeza sadaka ya kuteketezwa, na kuitoa sawasawa na sheria.

17. Kisha akaisongeza sadaka ya unga, na kutwaa konzi humo, na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi.

18. Huyo ng’ombe mume naye akamchinja, na huyo kondoo mume pia, dhabihu ya sadaka za amani, zilizokuwa kwa ajili ya watu; na wanawe Haruni wakamsongezea ile damu, naye akainyunyiza katika madhabahu pande zote,

19. na mafuta ya ng’ombe; na ya kondoo, mkia wake wa mafuta, na hayo yafunikayo matumbo, na figo zake, na kitambi cha ini;

Law. 9