6. Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa BWANA ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba.
7. Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yo yote ya utumishi.
8. Lakini mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
9. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
10. Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu;
11. naye atautikisa mganda mbele za BWANA ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa.
12. Na siku hiyo mtakayoutikisa mganda, mtamsongeza mwana-kondoo wa kiume mkamilifu wa mwaka wa kwanza awe sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA.