5. Nanyi hapo mtakapomchinjia BWANA sadaka ya amani mtaisongeza ili kwamba mpate kukubaliwa.
6. Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu cho chote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto.
7. Kwamba sadaka hiyo yaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa;
8. lakini kila mtu atakayekula atauchukua uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha BWANA; na nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
9. Na mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala usiyakusanye masazo ya mavuno yako;
10. wala usiyakusanye masazo ya mizabibu yako, wala usiyaokote matunda ya mizabibu yako yaliyopukutika; uyaache kwa ajili ya maskini na mgeni; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.
11. Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo.
12. Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi BWANA.
13. Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang’anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi.
14. Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi BWANA.
15. Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki.
16. Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; mimi ndimi BWANA.
17. Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake.
18. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA.
19. Mtazishika amri zangu. Usiwaache wanyama wako wa mfugo wakazaana kwa namna mbalimbali; usipande shamba lako mbegu za namna mbili pamoja; wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili zilizochanganywa pamoja.