1. BWANA akasema na Musa, baada ya kufa kwa hao wana wawili wa Haruni, walipokaribia mbele za BWANA, wakafa;
2. BWANA akamwambia Musa, Sema na Haruni ndugu yako, kwamba asiingie wakati wo wote katika mahali patakatifu ndani ya pazia, mbele ya kiti cha rehema, kilicho juu ya sanduku, asije akafa; maana, mimi nitaonekana katika lile wingu juu ya kiti cha rehema.
3. Haruni ataingia katika patakatifu na vitu hivi; ng’ombe mume mchanga kwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa.
4. Ataivaa ile kanzu takatifu ya kitani, atakuwa na zile suruali za kitani mwilini mwake, atafungwa ule mshipi wa kitani, naye atavaa ile kofia ya kitani; hayo ndiyo mavazi matakatifu, naye ataoga mwili wake majini, na kuyavaa.
5. Kisha atatwaa mikononi mwa mkutano wa Waisraeli mbuzi waume wawili, kwa sadaka ya dhambi; na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa.