Kut. 7:8-16 Swahili Union Version (SUV)

8. BWANA akanena na Musa na Haruni, akawaambia,

9. Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka.

10. Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama BWANA alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka.

11. Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao.

12. Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao.

13. Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama BWANA alivyonena.

14. BWANA akamwambia Musa, Moyo wa Farao ni mzito, anakataa kuwapa watu ruhusa waende zao.

15. Mwendee Farao asubuhi; tazama, atoka kwenda majini; nawe simama karibu na ufuo wa mto ili upate kuonana naye; na ile fimbo iliyogeuzwa kuwa nyoka utaichukua mkononi mwako.

16. Nawe umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani; nawe, tazama! Hujasikia hata sasa.

Kut. 7