Kut. 40:10-19 Swahili Union Version (SUV)

10. Kisha utaitia mafuta madhabahu ya kuteketeza sadaka, na vyombo vyake vyote; na kuiweka takatifu madhabahu; na hiyo madhabahu itakuwa takatifu sana.

11. Kisha utalitia mafuta birika na tako lake, na kuliweka liwe takatifu.

12. Kisha utamleta Haruni na wanawe hapo mlangoni pa hema ya kukutania, nawe utawaosha kwa maji.

13. Kisha utamvika Haruni mavazi matakatifu; nawe utamtia mafuta, na kumweka awe mtakatifu, ili apate kunitumikia katika kazi ya ukuhani.

14. Kisha utawaleta wanawe, na kuwavika kanzu zao;

15. nawe utawatia mafuta kama ulivyomtia mafuta baba yao, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani; na huko kutiwa mafuta kwao kutakuwa ni kwa ukuhani wa milele katika vizazi vyao vyote.

16. Musa akafanya hayo yote; kama yote BWANA aliyoagiza ndivyo alivyofanya.

17. Hata mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili, siku ya kwanza ya mwezi ile maskani ilisimamishwa.

18. Musa akaisimamisha maskani, akayaweka matako yake, akazisimamisha mbao zake akayatia mataruma yake, akazisimamisha nguzo zake.

19. Akaitanda hema juu ya maskani, akakitia kifuniko cha hema juu yake; kama BWANA alivyomwamuru Musa.

Kut. 40