Kut. 32:15-29 Swahili Union Version (SUV)

15. Basi, Musa akageuka akashuka katika mlima, na zile mbao mbili za mawe mikononi mwake; mbao zilizoandikwa pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa.

16. Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu nayo maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao.

17. Na Yoshua aliposikia kelele za watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni.

18. Akasema, Hiyo si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi.

19. Hata alipoyakaribia marago akaiona ile ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake, akazivunja chini ya mlima.

20. Akaitwaa ile ndama waliyoifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi, akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli.

21. Musa akamwambia Haruni Watu hawa wamekufanyani hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao?

22. Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake, wewe unawajua watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya.

23. Maana waliniambia, Katufanyie miungu, itakayokwenda mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata.

24. Nikawaambia, Mtu ye yote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu.

25. Basi Musa alipoona ya kuwa watu hawa wameasi, maana Haruni amewaacha waasi, ili wawe dhihaka kati ya adui zao,

26. ndipo Musa akasimama katika mlango wa marago, akasema, Mtu awaye yote aliye upande wa BWANA, na aje kwangu. Wana wa Lawi wote wakamkusanyikia

27. Akawaambia, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila mtu na ajifunge upanga wake pajani mwake, akapite huko na huko toka mlango hata mlango kati ya marago, mkamchinje kila mtu ndugu yake, na kila mtu mwenziwe na kila mtu jirani yake.

28. Na hao wana wa Lawi wakafanya kama vile alivyosema Musa, wakaanguka siku ile kama watu elfu tatu.

29. Musa akasema, Jiwekeni wakfu kwa BWANA leo, naam, kila mtu juu ya mwanawe na juu ya ndugu yake; ili awape baraka leo.

Kut. 32