10. Nao na wafanye sanduku la mti wa mshita; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu.
11. Nawe ulifunike kwa dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka pande zote.
12. Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande wake wa pili.
13. Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu.
14. Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku.
15. Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa.
16. Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa.
17. Nawe fanya kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa moja na nusu.
18. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku.
19. Weka kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku.
20. Na hayo makerubi yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha rehema.
21. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda nitakaokupa ndani ya sanduku.