Kut. 18:11-21 Swahili Union Version (SUV)

11. Sasa najua ya kuwa BWANA ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti.

12. Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu.

13. Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni.

14. Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni?

15. Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu;

16. wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake.

17. Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema.

18. Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako.

19. Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao;

20. nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya.

21. Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi;

Kut. 18