17. Wana wa Israeli wakafanya hivyo, wakaokota wengine zaidi, wengine kupungua.
18. Nao walipoipima kwa pishi, yeye aliyekuwa ameokota kingi hakubakiwa na kitu, na yeye aliyekuwa ameokota kichache hakupungukiwa; wakaokota kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa.
19. Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi.
20. Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana.
21. Basi wakaokota asubuhi baada ya asubuhi, kila mtu kama ulaji wake ulivyokuwa; na hapo jua lilipokuwa ni kali, kikayeyuka.
22. Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu maradufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa.
23. Akawaambia, Ndilo neno alilonena BWANA Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa BWANA; okeni mtakachooka, na kutokosa mtakachotokosa; na hicho kitakachowasalia jiwekeeni kilindwe hata asubuhi.
24. Basi wakakiweka hata asubuhi, kama Musa alivyowaagiza; nacho hakikutoa uvundo wala kuingia mabuu.
25. Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya BWANA; leo hamtakiona nje barani.
26. Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana.
27. Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione.
28. BWANA akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini?
29. Angalieni, kwa kuwa BWANA amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba.
30. Basi hao watu wakapumzika kwa siku ya saba.