Kum. 28:32-45 Swahili Union Version (SUV)

32. Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako.

33. Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima;

34. hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona.

35. BWANA atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa.

36. BWANA atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe.

37. Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza BWANA.

38. Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila.

39. Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu.

40. Utakuwa na mizeituni katika mipaka yako yote usijipake mafuta yake; kwa kuwa mzeituni wako utapukutika.

41. Utazaa wana na binti, lakini hawatakuwa wako wewe; kwa sababu watakwenda utumwani.

42. Miti yako yote, na mazao ya nchi yako, nzige watakuwa nayo.

43. Mgeni aliye kati yako atazidi kupaa juu yako; nawe utazidi kushuka chini.

44. Yeye atakukopesha, wala wewe usimkopeshe; yeye atakuwa ni kichwa, wewe utakuwa mkia.

45. Na laana hizi zote zitakujilia juu yako, zitakuandama na kukupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, kushika maagizo yake na amri zake alizokuagiza;

Kum. 28