1. Na itakuwa, ukiisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, iwe urithi, na kuimiliki, na kukaa ndani yake;
2. twaa malimbuko ya ardhi, utakayoyavuna katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako; ukayatie katika kikapu, ukaende hata mahali pale atakapopachagua BWANA, Mungu wako, ili alikalishe jina lake huko.
3. Ukamwendee kuhani atakayekuwapo siku zile, ukamwambie, Ninakiri leo kwa BWANA, Mungu wako, ya kuwa nimeingia katika nchi BWANA aliyowaapia baba zetu ya kwamba atatupa.
4. Naye kuhani atakipokea kikapu mkononi mwako, akiweke chini mbele ya madhabahu ya BWANA, Mungu wako.