1. Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo.
2. Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha BWANA.
3. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa BWANA, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.