1. Nisikilizeni, enyi visiwa; tegeni masikio yenu, enyi kabila za watu mlio mbali sana; BWANA ameniita tangu tumboni; toka tumbo la mama yangu amenitaja jina langu.
2. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha;
3. akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa.
4. Lakini nikasema, Nimejitaabisha bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida; lakini hakika hukumu yangu ina BWANA, na thawabu yangu ina Mungu wangu.