Isa. 24:4-18 Swahili Union Version (SUV)

4. Dunia inaomboleza, inazimia; ulimwengu unadhoofika, unazimia; watu wakuu wa dunia wanadhoofika.

5. Tena dunia imetiwa unajisi kwa watu wanaoikaa; kwa maana wameziasi sheria, wameibadili amri, wamelivunja agano la milele.

6. Ndiyo sababu laana imeila dunia hii, na hao wanaoikaa wameonekana kuwa na hatia, ndiyo sababu watu wanaoikaa dunia wameteketea, watu waliosalia wakawa wachache tu.

7. Divai mpya inaomboleza, mzabibu umedhoofika, watu wote waliochangamka moyo wanaugua.

8. Sauti ya furaha ya matoazi inakoma; kelele yao wafurahio imekwisha; furaha ya kinubi inakoma.

9. Hawatakunywa divai pamoja na nyimbo; kileo kitakuwa uchungu kwao wakinywao.

10. Mji wa machafuko umebomolewa; kila nyumba imefungwa, asipate kuingia mtu awaye yote.

11. Pana kilio katika njia kuu kwa sababu ya divai; furaha yote imetiwa giza, na changamko la nchi limetoweka.

12. Ndani ya mji umebaki ukiwa, na lango lake limepigwa kwa uharibifu.

13. Maana katikati ya dunia, katikati ya mataifa, itakuwa hivi; kama wakati utikiswapo mzeituni, kama wakati waokotapo zabibu baada ya mavuno yake.

14. Hawa watainua sauti zao, watapiga kelele; kwa sababu ya utukufu wa BWANA watapiga kelele toka baharini.

15. Basi, mtukuzeni BWANA katika mashariki, litukuzeni jina la BWANA, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari.

16. Toka pande za mwisho wa dunia tumesikia nyimbo, Atukuzwe mwenye haki. Ndipo niliposema, Kukonda kwangu! Kukonda kwangu! Ole wangu! Watenda hila wametenda hila, naam, watendao hila wametenda hila sana.

17. Hofu, na shimo, na mtego, vi juu yako, Ee mwenye kukaa duniani.

18. Itakuwa kila akimbiaye sauti ya hofu ataanguka katika shimo; na kila apandaye na kutoka shimoni atanaswa na mtego; kwa maana madirisha yaliyo juu yamewekwa wazi, na misingi ya dunia inatikisika.

Isa. 24