1. Njoni, tumrudie BWANA; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu.
2. Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake.
3. Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua BWANA; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi.
4. Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema.