6. kisha atatia juu yake ngozi za pomboo za kulifunikia, na kutandika juu yake nguo ya rangi ya samawi tupu, kisha watatia hiyo miti yake.
7. Tena juu ya meza ya mikate ya wonyesho watatandika nguo ya rangi ya samawi, na kuweka juu yake sahani, na miiko, na mabakuli, na vikombe vya kumiminia; na hiyo mikate ya daima itakuwa juu yake;
8. nao watatandika juu yake nguo ya rangi nyekundu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo za kuifunikia, na kuitia ile miti yake.
9. Kisha watatwaa nguo ya rangi ya samawi, na kukifunika kinara cha taa ya nuru, na taa zake, na makasi yake, na sahani zake za kutilia makaa, na vyombo vyake vyote vya mafuta, watumiavyo kwa kazi yake;
10. nao watakitia, na vyombo vyake vyote, ndani ya ngozi ya pomboo, na kukitia juu ya miti ya kukichukulia
11. Tena watatandika nguo ya rangi ya samawi juu ya madhabahu ya dhahabu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo, na kuitia ile miti yake;