11. Tena watatandika nguo ya rangi ya samawi juu ya madhabahu ya dhahabu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo, na kuitia ile miti yake;
12. kisha watavitwaa vile vyombo vyote vya utumishi wavitumiavyo katika mahali patakatifu, na kuvitia katika nguo ya rangi ya samawi, na kuvifunika kwa ngozi za pomboo, na kuvitia juu ya miti ya kuvichukulia.
13. Nao watayaondoa hayo majivu madhabahuni; na kutandika nguo ya rangi ya zambarau juu yake;
14. nao wataweka vyombo vyake vyote juu yake ambavyo wavitumia katika madhabahu, vyetezo, na nyuma, na miiko, na mabakuli, vyombo vyote vya hiyo madhabahu; nao watatandika juu yake ngozi za pomboo, na kutia miti yake mahali pake.
15. Na Haruni na wanawe watakapokwisha kupafunika mahali patakatifu, na vyombo vyote vya mahali patakatifu, hapo watakapong’oa kambi; baadaye, wana wa Kohathi watakuja kuvichukua; lakini wasiviguse vile vitu vitakatifu, wasife. Vyombo vile ni mzigo wa wana wa Kohathi katika hema ya kukutania.
16. Na ulinzi wake Eleazari mwana wa Haruni kuhani utakuwa ni kuyaangalia mafuta kwa nuru, na uvumba mzuri, na sadaka ya unga ya daima, na mafuta ya kupaka, tena ulinzi wa hiyo maskani yote, na wa vitu vyote vilivyo ndani yake, mahali patakatifu, na vyombo vyake.
17. Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
18. Msiitenge kabisa kabila ya jamaa za Wakohathi katika hao Walawi;
19. lakini wafanyieni neno hili, ili kwamba wawe hai, wasife, hapo watakapovikaribia vile vitu vilivyo vitakatifu sana; Haruni na wanawe wataingia ndani, na kuwawekea kila mtu utumishi wake, na kila mtu mzigo wake;
20. lakini wasiingie wao kupaona mahali pale patakatifu, hata kwa dakika moja, ili wasife.
21. Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
22. Fanya jumla ya wana wa Gershoni nao, kwa nyumba za baba zao, na jamaa zao;
23. tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini utawahesabu; wote watakaoingia kutumika, ili kufanya kazi katika hema ya kukutania.
24. Huu ni utumishi wa jamaa za Wagershoni, katika kutumika na katika kuchukua mizigo;
25. wao watayachukua mapazia ya maskani, na hema ya kukutania, hizo nguo za kufunikia, na zile ngozi za pomboo za kufunikia zilizo juu yake, na pazia la mlango wa hema ya kukutania;
26. na kuta za nguo za ua, na sitara ya ile nafasi ya kuingilia ya lango la ua, ulio karibu na maskani na madhabahu, kuzunguka pande zote, na kamba zake, na vyombo vyote vya utumishi wao, na yote yatakayotendeka kwavyo, watatumika katika hayo.
27. Utumishi wote wa wana wa Wagershoni, katika mzigo wao wote, na utumishi wao wote, utakuwa kwa amri ya Haruni na wanawe; nanyi mtawaagizia mzigo wao wote kuulinda.
28. Huu ni utumishi wa jamaa za wana wa Wagershoni katika hema kukutania; na ulinzi utakuwa chini ya mkono wa Ithamari mwana wa Haruni kuhani.
29. Katika habari ya wana wa Merari, utawahesabu kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao;