1. Kisha hao watu walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa BWANA; BWANA aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa BWANA ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago.
2. Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba BWANA, na ule moto ukakoma.
3. Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa BWANA ukawaka kati yao.
4. Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule?
5. Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;
6. lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu.
7. Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola.
8. Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya.
9. Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao.