Eze. 45:10-23 Swahili Union Version (SUV)

10. Mtakuwa na mizani ya haki, na efa ya haki, na bathi ya haki.

11. Efa na bathi zitakuwa za kipimo kimoja; ili kwamba bathi ichukue sehemu ya kumi ya homeri, na efa sehemu ya kumi ya homeri; kipimo chake kitakuwa kwa kadiri ya cheo cha kawaida cha homeri.

12. Nayo shekeli itakuwa gera ishirini; shekeli tano zitakuwa shekeli tano, shekeli kumi zitakuwa kumi, na shekeli hamsini zitakuwa mane yenu.

13. Toleo mtakalotoa ni hili; sehemu ya sita ya efa katika homeri moja ya ngano, nanyi mtatoa sehemu ya sita ya efa katika homeri ya shayiri;

14. na sehemu ya mafuta iliyoamriwa, katika bathi ya mafuta, itakuwa sehemu ya kumi ya bathi katika kori moja, ambayo ni bathi kumi, yaani homeri; maana bathi kumi ni homeri moja;

15. na mwana-kondoo mmoja wa kundi katika mia mbili, katika malisho ya Israeli yenye maji; kwa sadaka ya unga, na kwa sadaka ya kuteketezwa, na kwa sadaka za amani, ili kuwafanyia upatanisho, asema Bwana MUNGU.

16. Watu wote wa nchi watatoa toleo hili kwa ajili ya mkuu katika Israeli.

17. Tena itakuwa kazi ya mkuu kutoa hizo sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na sadaka za vinywaji, katika sikukuu, na katika mwezi mpya, na katika sabato, katika sikukuu zote za nyumba ya Israeli zilizoamriwa; atatengeneza sadaka ya dhambi, na sadaka ya unga, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ya Israeli.

18. Bwana MUNGU asema hivi; Mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, utatwaa ng’ombe mchanga mume mkamilifu; nawe utapatakasa mahali patakatifu.

19. Na kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya dhambi, na kuitia juu ya miimo ya milango ya nyumba, na juu ya pembe nne za daraja ya madhabahu, na juu ya miimo ya lango la ua wa ndani.

20. Nawe utafanya vivyo hivyo katika mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi kwa ajili ya kila mtu akosaye, na kwa ajili ya mtu aliye mjinga, ndivyo mtakavyoifanyia nyumba upatanisho.

21. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, mtakuwa na Pasaka, sikukuu ya siku saba; mkate usiotiwa chachu utaliwa.

22. Na siku hiyo mkuu atatengeneza ng’ombe kuwa sadaka ya dhambi, kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu wote wa nchi.

23. Tena, katika zile siku saba za sikukuu atamtengenezea BWANA sadaka ya kuteketezwa, ng’ombe saba na kondoo waume saba wakamilifu, kila siku kwa muda wa siku saba, na beberu mmoja kila siku kuwa sadaka ya dhambi.

Eze. 45