13. Sheba, na Dedani, na wafanya biashara wa Tarshishi, pamoja na wana-simba wake wote, watakuambia, Je! Umekuja kuteka mateka? Umekusanya jeshi lako, ili kuwinda mawindo? Kuchukua fedha na dhahabu, kuchukua ng’ombe na mali, kuteka mateka mengi sana?
14. Basi, mwanadamu, tabiri, umwambie Gogu, Bwana MUNGU asema hivi; Katika siku ile watu wangu, Israeli, watakapokaa salama, hutapata habari?
15. Nawe utakuja kutoka mahali pako, kutoka pande za mwisho za kaskazini, wewe, na watu wa kabila nyingi pamoja nawe, wote wamepanda farasi, kusanyiko kubwa, na jeshi kuu;
16. nawe utapanda juu uwajilie watu wangu, Israeli, kama wingu kuifunika nchi; itakuwa katika siku za mwisho, nitakuleta upigane na nchi yangu, ili mataifa wanijue, nitakapotakaswa kwako, Ewe Gogu, mbele ya macho yao.