24. Mwanadamu, watu wale wakaao mahali palipoharibika katika nchi ya Israeli husema ya kwamba, Ibrahimu alikuwa mmoja, akairithi nchi hii; lakini sisi tu watu wengi; tumepewa nchi hii iwe urithi wetu.
25. Basi, waambie, Bwana MUNGU asema hivi; Mnakula nyama pamoja na damu yake, na kuviinulia vinyago vyenu macho yenu, na kumwaga damu; je, mtaimiliki nchi hii?
26. Mnategemea upanga wenu, mnatenda machukizo, mnanajisi kila mtu mke wa jirani yake; je! Mtaimiliki nchi hii?
27. Hivi ndivyo utakavyowaambia, Bwana MUNGU asema hivi; Kama mimi niishivyo, hakika watu wale wakaao mahali palipoharibika wataanguka kwa upanga, naye mtu aliye katika uwanda, nitamtoa na kuwapa wanyama wakali, ili aliwe; na hao walio ndani ya ngome na mapango watakufa kwa tauni.
28. Nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa na ajabu, na kiburi cha uwezo wake kitakoma; nayo milima ya Israeli itakuwa ukiwa, asipite mtu.