17. Nao watakufanyia maombolezo, na kukuambia, Imekuwaje wewe kuharibika, wewe uliyekaliwa na wana-maji, mji wenye sifa, uliyekuwa na nguvu katika bahari, mji huo, na hao waliokaa ndani yake, waliowatia hofu wote waliokaa ndani yake!
18. Sasa visiwa vitatetemeka katika siku ya kuanguka kwako; naam, visiwa vilivyo katika bahari vitafadhaika, kwa sababu ya kuondoka kwako.
19. Maana Bwana MUNGU asema hivi; Nitakapokufanya kuwa mji wa ukiwa, kama miji isiyokaliwa na watu; nitakapoleta vilindi vya bahari juu yako, na maji makuu yatakapokufunika;
20. ndipo nitakapokushusha pamoja nao washukao shimoni, uende kwa watu wa kale; nami nitakukalisha pande za chini za nchi; mahali palipokuwa ukiwa tangu zamani, pamoja nao washukao shimoni; ili usikaliwe na watu, wala usiweke utukufu wako katika nchi yao walio hai.
21. Nitakufanya kuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwako tena; ujapotafutwa, lakini hutaonekana tena kabisa, asema Bwana MUNGU.