Eze. 22:14-26 Swahili Union Version (SUV)

14. Je! Moyo wako waweza kuvumilia, au mkono wako waweza kuwa hodari, katika siku zile nitakapokutenda mambo? Mimi, BWANA, nimenena neno hili, tena nitalitenda.

15. Nami nitakutawanya kati ya mataifa, na kukutapanya kati ya nchi mbalimbali; nami nitauteketeza uchafu wako, ili ukutoke.

16. Nawe utatiwa unajisi ndani ya nafsi yako, mbele ya macho ya mataifa; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.

17. Neno la BWANA likanijia, kusema,

18. Mwanadamu, nyumba ya Israeli imekuwa taka za fedha kwangu; wote wamekuwa shaba, na bati, na chuma, na risasi, kati ya tanuu; wamekuwa taka za fedha.

19. Basi Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu ninyi nyote mmekuwa taka za fedha, tazama, nitawakusanya kati ya Yerusalemu.

20. Kama vile watu wakusanyavyo fedha, na shaba, na chuma, na risasi, na bati, kati ya tanuu, ili kuvifukutia moto na kuviyeyusha; ndivyo nitakavyowakusanya ninyi katika hasira yangu, na ghadhabu yangu, nami nitawalaza huko, na kuwayeyusha.

21. Naam, nitawakusanya, na kuwafukutia moto wa ghadhabu yangu, nanyi mtayeyushwa kati yake.

22. Kama fedha iyeyushwavyo kati ya tanuu, ndivyo mtakavyoyeyushwa kati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, nimemwaga ghadhabu yangu juu yenu.

23. Neno la BWANA likanijia, kusema,

24. Mwanadamu, uiambie nchi, Wewe u nchi isiyosafika, wala kunyeshewa mvua siku ya ghadhabu.

25. Fitina ya manabii wake imo ndani yake, kama simba angurumaye akirarua mawindo; wamekula roho za watu; hutwaa kwa nguvu hazina na vitu vya thamani; wameongeza hesabu ya wajane wake ndani yake.

26. Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao.

Eze. 22