3. Nao maakida wa majimbo, na majumbe, na maliwali, na wale waliofanya shughuli ya mfalme, waliwasaidia Wayahudi; kwa sababu hofu ya Mordekai imewaangukia.
4. Maana Mordekai alikuwa mkuu nyumbani mwa mfalme, na sifa yake imevuma katika majimbo yote, kwa kuwa huyo Mordekai amezidi kukuzwa.
5. Basi Wayahudi wakawapiga adui zao wote mapigo ya upanga, na machinjo, na maangamizo, wakawatenda kama wapendavyo wale waliowachukia.
6. Hata huko Shushani ngomeni Wayahudi wakawaua watu mia tano, na kuwaangamiza.
7. Wakawaua na Parshandatha, na Dalfoni, na Aspatha,
8. na Poratha, na Adalia, na Aridatha,
9. na Parmashta, na Arisai, na Aridai, na Waizatha,
10. wana kumi wa Hamani bin Hamedatha, adui ya Wayahudi; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono.
11. Siku ile mfalme akaletewa hesabu ya hao waliouawa huko Shushani ngomeni.
12. Mfalme akamwambia malkia Esta, Wayahudi wamewaua watu mia tano hapa Shushani ngomeni na kuwaangamiza, pamoja na wana kumi wa Hamani, je! Wamefanyaje basi katika majimbo ya mfalme yaliyosalia! Basi, una nini uombalo? Nawe utapewa; ama unayo haja gani tena? Nayo itatimizwa.
13. Ndipo Esta aliposema, Mfalme akiona vema, Wayahudi walioko Shushani na wapewe ruhusa kufanya tena kesho sawasawa na mbiu ya leo, na hao wana kumi wa Hamani watundikwe juu ya mti ule.
14. Mfalme akaamuru vifanyike vivyo hivyo, mbiu ikapigwa huko Shushani, wakawatundika wale wana kumi wa Hamani.