Dan. 8:9-24 Swahili Union Version (SUV)

9. Na katika moja ya pembe hizo ilitokea pembe ndogo, iliyokua sana, upande wa kusini, na upande wa magharibi, na upande wa nchi ya uzuri.

10. Nayo ikakua, kiasi cha kulifikilia jeshi la mbinguni; ikaangusha chini baadhi ya jeshi lile, na ya nyota, ikazikanyaga.

11. Naam, ikajitukuza hata juu yake aliye mkuu wa jeshi hilo, ikamwondolea sadaka ya kuteketezwa ya daima, na mahali pa patakatifu pake pakaangushwa chini.

12. Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa.

13. Ndipo nikamsikia mtakatifu mmoja akinena, na mtakatifu mwingine akamwuliza huyo aliyenena, Haya maono katika habari ya sadaka ya kuteketezwa ya daima, na lile kosa lifanyalo ukiwa, yataendelea hata lini, kukanyagisha patakatifu na jeshi?

14. Akamwambia, Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa.

15. Ikawa mimi, naam, mimi Danieli, nilipoyaona maono hayo, nalitafuta kuyafahamu, na tazama, alisimama mbele yangu mmoja mfano wa mwanadamu.

16. Nikasikia sauti ya mwanadamu katikati ya mto Ulai, iliyoita na kusema, Gabrieli, mfahamishe mtu huyu maono haya.

17. Basi alipakaribia mahali niliposimama; nami naliogopa alipokaribia, nikaanguka kifudifudi; lakini aliniambia, Fahamu, Ee mwanadamu, kwa maana maono haya ni ya wakati wa mwisho.

18. Basi alipokuwa akisema nami, nalishikwa na usingizi mzito na uso wangu uliielekea nchi; lakini alinigusa, akanisimamisha wima.

19. Akaniambia, Tazama, nitakujulisha yatakayokuwa wakati wa mwisho wa ghadhabu; maana, ni ya wakati wa mwisho ulioamriwa.

20. Yule kondoo mume uliyemwona, mwenye pembe mbili, hizo ndizo wafalme wa Umedi na Uajemi.

21. Na yule beberu, mwenye manyoya mengi, ni mfalme wa Uyunani; na ile pembe kubwa iliyo kati ya macho yake ni mfalme wa kwanza.

22. Tena katika habari ya pembe ile iliyovunjika, ambayo badala yake zilisimama pembe nne, falme nne zitasimama kutoka katika taifa lile, lakini si kwa nguvu kama zake.

23. Na wakati wa mwisho wa ufalme wao, wakosao watakapotimia, mfalme mwenye uso mkali, afahamuye mafumbo, atasimama.

24. Na nguvu zake zitakuwa nyingi mno, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe; naye ataharibu kiasi cha kustaajabisha watu, na kufanikiwa, na kutenda apendavyo; naye atawaangamiza hao walio hodari na watu watakatifu.

Dan. 8