26. Mfalme akajibu, akamwambia Danieli, aliyekuwa akiitwa Belteshaza, Je! Waweza kunijulisha ile ndoto niliyoiona, na tafsiri yake.
27. Danieli akajibu mbele ya mfalme, akasema, Ile siri aliyoiuliza mfalme, wenye hekima hawawezi kumfunulia mfalme; wala wachawi, wala waganga, wala wanajimu;
28. lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadreza mambo yatakayokuwa siku za mwisho.Ndoto yako, na njozi za kichwa chako ulizoziona kitandani pako, ni hizi;
29. Wewe, Ee mfalme, mawazo yako yaliingia moyoni mwako kitandani pako ya mambo yatakayokuwa halafu; na yeye afunuaye siri amekujulisha mambo yatakayokuwa.
30. Lakini mimi, sikufunuliwa siri hii kwa sababu ya hekima iwayo yote niliyo nayo zaidi ya watu wengine walio hai, bali kusudi mfalme afunuliwe ile tafsiri, nawe upate kujua mawazo ya moyo wako.