Ayu. 9:20-31 Swahili Union Version (SUV)

20. Ingawa ni mwenye haki, kinywa changu mwenyewe kitanihukumu;Ingawa ni mkamilifu, kitanishuhudia kuwa ni mpotovu.

21. Mimi ni mkamilifu; siangalii nafsi yangu;Naudharau uhai wangu.

22. Hayo yote ni mamoja; kwa hiyo nasema,Yeye huangamiza wakamilifu na waovu pia.

23. Kama hilo pigo likiua ghafula,Atayadhihaki majaribu yake asiye na kosa.

24. Dunia imetiwa mkononi mwa waovu;Yeye hufunika nyuso za waamuzi wake;Kama si yeye, ni nani basi?

25. Basi siku zangu zina mbio kuliko tarishi;Zakimbia, wala hazioni mema.

26. Zimepita kama merikebu ziendazo mbio;Mfano wa tai ayashukiaye mawindo.

27. Nikisema, Mimi nitasahau kuugua kwangu,Nitaacha kununa uso nikachangamke moyo;

28. Mimi huziogopa huzuni zangu zote,Najua kuwa hutanihesabu kuwa sina hatia.

29. Nitahukumiwa kuwa ni mkosa;Ya nini basi nitaabike bure?

30. Ingawaje najiosha kwa maji ya theluji,Na kuitakasa mikono yangu kwa sabuni;

31. Lakini utanitupa shimoni,Nami hata nguo zangu zitanichukia.

Ayu. 9