Ayu. 41:19-27 Swahili Union Version (SUV)

19. Mienge iwakayo hutoka kinywani mwake,Na macheche ya moto huruka nje.

20. Moshi hutoka katika mianzi ya pua yake,Kama nyungu ikitokota, na manyasi yawakayo.

21. Pumzi zake huwasha makaa,Na miali ya moto hutoka kinywani mwake.

22. Katika shingo yake hukaa nguvu,Na utisho hucheza mbele yake.

23. Manofu ya nyama yake hushikamana;Yanakazana juu yake; hayawezi kuondolewa.

24. Moyo wake una imara kama jiwe;Naam, imara kama jiwe la chini la kusagia.

25. Anapojiinua, mashujaa huogopa;Kwa sababu ya woga wao huvunjwa moyo.

26. Mtu akimpiga kwa upanga, haumwingii;Wala fumo, wala mshale, wala mkuki wenye ncha.

27. Yeye huona chuma kuwa kama nyasi,Na shaba kama mti uliooza.

Ayu. 41