1. Tazama, jicho langu limeyaona hayo yote,Sikio langu limeyasikia na kuelewa nayo.
2. Hayo myajuayo ninyi, na mimi pia nayajua;Mimi si duni kuliko ninyi.
3. Hakika ningenena naye huyo Mwenyezi,Nami nataka kuhojiana na Mungu.
4. Lakini ninyi hubuni maneno ya uongo,Ninyi nyote ni matabibu wasiofaa.
5. Laiti mngenyamaza kabisa!Hilo lingekuwa hekima kwenu.
6. Sikieni sasa basi hoja zangu,Mkayasikie mashindano ya midomo yangu.
7. Je! Mtanena yasiyo ya haki kwa ajili ya Mungu,Na kusema kwa udanganyifu kwa ajili yake?
8. Je! Mtamwonyesha yeye upendeleo?Mtamtetea Mungu?
9. Je! Itafaa yeye kuwatafuta ninyi?Au, kama kumdanganya mtu, je! Mtamdanganya yeye?
10. Hakika atawakemea ninyi,Mkiwapendelea watu kwa siri.
11. Je! Huo ukuu wake hautawatia hofu,Na utisho wake hautawaangukia?
12. Matamko yenu ya hekima ni mithali ya majivu,Ngome zenu ni ngome za udongo.
13. Nyamazeni, niacheni, ili nipate kunena,Na hayo yatakayonijilia na yaje.
14. Nitaitwaa nyama ya mwili wangu katika meno yangu,Na kuutwaa uhai wangu mkononi mwangu!
15. Tazama, ataniua; sina tumaini;Ila hata hivyo nitaithibitisha njia yangu mbele yake.
16. Hili nalo litakuwa ni wokovu wangu;Kwani asiyemcha Mungu hatakaribia mbele yake.
17. Sikieni sana maneno yangu,Maelezo yangu na yaingie masikioni mwenu.