21. Ndipo hapo Zeba na Salmuna wakasema, Simama wewe ukatuangukie sisi; kwa maana kama mtu alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake. Basi Gideoni akasimama, akawaua Zeba na Salmuna, akazitwaa koja zilizokuwa katika shingo za ngamia zao.
22. Ndipo watu wa Israeli wakamwambia Gideoni, Tawala wewe juu yetu, wewe, na mwanao, na mjukuu wako pia; kwa kuwa wewe umetuokoa na mikono ya Midiani.
23. Gideoni akawaambia, Mimi sitatawala juu yenu wala mwanangu hatatawala juu yenu; yeye BWANA atatawala juu yenu.
24. Kisha Gideoni akawaambia, Mimi nina haja yangu niitakayo kwenu, ni ya kila mtu kunipa hizo pete za masikio ya mateka yake. (Kwa maana walikuwa na pete za masikio za dhahabu, kwa sababu walikuwa ni Waishmaeli.)