Amu. 7:5-11 Swahili Union Version (SUV)

5. Basi akawaleta watu chini majini. BWANA akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa.

6. Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji.

7. BWANA akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake.

8. Basi wale watu wakachukua vyakula vyao mikononi mwao, na tarumbeta zao; naye akawapeleka watu wote wa Israeli, kila mtu hemani kwake; bali aliwazuia wale watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni.

9. Ikawa usiku uo huo BWANA akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako.

10. Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini;

11. nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hata kufikilia mwisho wa watu wenye silaha waliokuwa kambini.

Amu. 7