Amu. 15:13-20 Swahili Union Version (SUV)

13. Wakamwambia, wakisema, Vema, lakini tutakufunga sana, na kukutia katika mikono yao; lakini hakika hatutakuua. Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakamchukua kutoka huko jabalini.

14. Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya BWANA ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake.

15. Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo;

16. Samsoni akasema,Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu,Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu.

17. Ikawa, alipokuwa amekwisha kunena akautupa ule mfupa wa taya mkononi mwake; na mahali pale pakaitwa Ramath-lehi.

18. Kisha akaona kiu sana, akamwita BWANA akasema, Wewe umetupa wokovu huu kwa mkono wa mtumishi wako; na sasa nitakufa kwa kiu, na kuanguka katika mikono ya watu wasiotahiriwa.

19. Lakini Mungu akapasua mahali penye shimo palipo katika Lehi, pakatoka maji; naye alipokwisha kunywa, roho yake ikamrudia, akaburudika; kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Enhakore, napo pa katika Lehi hata hivi leo.

20. Naye akawa mwamuzi wa Israeli: katika siku za Wafilisti muda wa miaka ishirini.

Amu. 15