1. Samsoni akatelemkia Timna, akaona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti.
2. Kisha akapanda, akawaambia baba yake na mama yake, akasema, Nimemwona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti; basi mnipatie, nimwoe.
3. Ndipo baba yake na mama yake wakamwambia, Je! Hapana mwanamke hata mmoja katika ndugu zako, au katika jamaa zangu zote, hata uende kumwoa mwanamke kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa? Samsoni akamwambia baba yake; Mnipatie huyo, kwa maana ananipendeza sana.
4. Lakini baba yake na mama yake hawakujua ya kuwa jambo hili ni la BWANA; maana alitaka kisa juu ya Wafilisti. Basi wakati ule Wafilisti walikuwa wakiwatawala Israeli.
5. Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia.
6. Roho ya BWANA ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.