1. Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.
2. Ndipo mfalme akawaita Wagibeoni akawaambia; (basi Wagibeoni si wa wana wa Israeli, ila ni wa masalio ya Waamori; na wana wa Israeli walikuwa wamewaapia; lakini Sauli akatafuta kuwaua katika juhudi yake kwa ajili ya wana wa Israeli na Yuda;)
3. basi Daudi akawaambia hao Wagibeoni, Niwatendee nini? Na kwa tendo gani nifanye upatanisho, mpate kuubariki urithi wa BWANA?
4. Na hao Wagibeoni wakamwambia, Si jambo la fedha wala dhahabu lililo kati ya sisi na Sauli, au nyumba yake; wala si juu yetu kumwua mtu ye yote katika Israeli. Akasema Mtakayoyanena, ndiyo nitakayowatendea ninyi.
5. Wakamwambia mfalme, Yule mtu aliyetupoteza, na kutufanyia shauri la kutuharibu, tusikae katika mipaka yo yote ya Israeli,
6. basi, na tutolewe watu saba katika wanawe, nasi tutawatundika mbele za BWANA katika Gibeoni, katika mlima wa BWANA. Mfalme akasema, Nitawatoa.