10. Wala Amasa hakuangalia huo upanga uliomo mkononi mwa Yoabu; basi akampiga nao wa tumbo, akamwaga matumbo yake chini, asimpige mara ya pili; naye akafa. Kisha Yoabu na Abishai, nduguye, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri.
11. Akasimama karibu naye mmojawapo wa vijana wa Yoabu, huyo akasema, Ampendaye Yoabu, na aliye wa Daudi, na amfuate Yoabu.
12. Lakini Amasa alikuwa anagaagaa katika damu yake katikati ya njia kuu. Basi yule mtu alipowaona watu wote wamesimama, akamwondoa Amasa toka njia kuu akamtia kondeni, akamfunika nguo, hapo alipoona ya kuwa kila mtu aliyefika kwake amesimama.
13. Na alipoondolewa katika njia kuu, watu wote wakapita, wakamwandama Yoabu ili kumfuatia Sheba, mwana wa Bikri.
14. Naye akapita kati ya kabila zote za Israeli mpaka Abeli, na kwa Bethmaaka na Wabikri wote; nao wakakusanyika, wakaenda pia kumwandama.
15. Na hao wakaja wakamhusuru katika Abeli wa Bethmaaka, wakafanya chuguu mbele ya mji, nayo ikasimama kuielekea ngome; na watu wote waliokuwa pamoja na Yoabu wakavunja-vunja ukuta, wapate kuubomoa.
16. Ndipo akalia mwanamke mmoja mwenye akili toka mjini, Sikieni, sikieni; mwambieni na Yoabu, aje hapa karibu, niseme naye.
17. Basi akamkaribia; na yule mwanamke akasema, Ndiwe Yoabu? Akajibu, Ndimi. Ndipo akamwambia Sikia maneno ya mjakazi wako. Akajibu, Mimi nasikia.
18. Kisha akanena, akisema, Watu hunena zamani za kale, wakisema, Wasikose kuuliza huko Abeli; ndivyo walivyomaliza shauri.
19. Mimi ni wa hao wenye amani, walio waaminifu katika Israeli; wewe unatafuta kuuharibu mji, na mama wa Israeli; mbona wataka kuumeza urithi wa BWANA?
20. Yoabu akajibu, akasema, Isiwe, isiwe kwangu, niumeze wala kuuharibu.
21. Neno hili silo hivyo; lakini mtu mmoja wa milima ya Efraimu, Sheba, mwana wa Bikri, jina lake, ameinua mkono wake juu ya mfalme, naam, Daudi, basi mtoeni yeye tu, nami nitaondoka katika mji huu. Basi yule mwanamke akamwambia Yoabu, Tazama, kichwa chake utatupiwa juu ya ukuta.