1. Basi ilitukia ya kwamba kulikuwapo mtu asiyefaa, jina lake akiitwa Sheba, mwana wa Bikri, Mbenyamini; naye akapiga tarumbeta, akasema, Sisi hatuna sehemu katika Daudi, wala hatuna urithi katika mwana wa Yese; nendeni kila mtu hemani kwake, enyi Israeli.
2. Basi wakapanda watu wote wa Israeli kutoka kumfuata Daudi, wakamfuata Sheba, mwana wa Bikri; lakini watu wa Yuda wakaambatana na mfalme wao, toka Yordani hata kufika Yerusalemu.
3. Basi Daudi akaja Yerusalemu nyumbani kwake; kisha mfalme akawatwaa wale wanawake kumi, masuria, aliowaacha kuitunza nyumba, akawatia nyumbani mwa kulindwa, akawalisha, ila asiingie kwao. Basi wakafungwa hata siku ya kufa kwao, huku wakiishi hali ya ujane.
4. Ndipo mfalme akamwambia Amasa, Uwakusanye pamoja kwangu kwa siku tatu watu wa Yuda, na uwepo wewe hapa.
5. Amasa akaenda kuwakusanya Yuda; lakini akakawia zaidi ya huo muda aliowekewa.
6. Basi Daudi akamwambia Abishai, Sasa Sheba, mwana wa Bikri, atatudhuru, kuliko Absalomu; twaa wewe watumishi wa bwana wako, ukamfuatie, asiingie katika miji yenye boma, na kujiponya machoni petu.