16. Akafanya haraka Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu akashuka pamoja na watu wa Yuda ili kumlaki mfalme Daudi.
17. Na Watu elfu wa Benyamini walikuwa pamoja naye, na huyo Siba mtumwa, nyumba ya Sauli, na hao wanawe kumi na watano, na watumwa wake ishirini pamoja naye; wakavuka Yordani mbele ya mfalme.
18. Tena ikavuka mashua ili kuwavusha jamaa ya mfalme, na kufanya aliyoyaona kuwa mema.Ndipo Shimei, mwana wa Gera, akamwangukia mfalme alipokuwa amevuka Yordani.
19. Akamwambia mfalme, Bwana wangu asinihesabie uovu, wala usiyakumbuke yale niliyoyatenda mimi mtumwa wako kwa upotoe siku ile alipotoka Yerusalemu bwana wangu mfalme, hata mfalme ayatie moyoni mwake.