21. Na mfalme Daudi alipoyasikia maneno hayo yote, alikasirika sana.
22. Ila Absalomu hakusema na Amnoni wala kwa heri wala kwa shari; kwa maana Absalomu alimchukia Amnoni kwa kumtenza nguvu umbu lake Tamari.
23. Ikawa baada ya miaka miwili mizima, Absalomu alikuwa na wenye kukata manyoya ya kondoo huko Baal-hasori uliopo upande wa Efraimu; naye Absalomu akawaalika wana wote wa mfalme.
24. Absalomu akamjia mfalme, akasema, Tazama sasa, mimi mtumwa wako ninao wakata manyoya ya kondoo; basi mfalme na aende, nakusihi, na watumishi wake pamoja nami mtumwa wako.
25. Mfalme akamwambia Absalomu, Sivyo, mwanangu, tusiende sote, tusije tukakulemea. Akamsihi sana; asikubali kwenda, ila akambariki.
26. Ndipo akasema Absalomu, Kwamba huji, nakusihi, mwache ndugu yangu Amnoni aende nasi.
27. Mfalme akamwambia, Kwa nini aende nawe? Lakini Absalomu akamsihi sana, naye akamwacha Amnoni na wana wote wa mfalme waende naye.
28. Kisha Absalomu akawaamuru watumishi wake, akasema, Angalieni basi, moyo wake Amnoni utakapofurahiwa kwa mvinyo; nami nitakapowaambia, Mpigeni Amnoni, ndipo mwueni, msiogope; si mimi niliyewaamuru? Iweni hodari, iweni na ujasiri.
29. Basi watumishi wa Absalomu wakamfanyia Amnoni kama alivyoamuru Absalomu. Ndipo wakaondoka wana wote wa mfalme, wakapanda kila mtu nyumbu wake, wakakimbia.
30. Ikawa, walipokuwa njiani, habari zikamwasilia Daudi, kusema, Absalomu amewaua wana wote wa mfalme, wala hata mmoja wao hakusalia.