1. Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu.
2. Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho.
3. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti?
4. Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.
5. Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito.
6. Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria, Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi.
7. Uria alipomwendea Daudi, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, na habari za watu, na habari za vita.
8. Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme.