11. Na manabii wote wakatoa unabii huo, wakisema, Kwea Ramoth-gileadi, ukafanikiwe, kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme.
12. Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja yasema mema kwa mfalme; neno lako basi na liwe kama mojawapo lao, ukaseme mema.
13. Mikaya akasema, Kama aishivyo BWANA, neno lile atakalolinena Mungu wangu, ndilo nitakalolinena.
14. Na alipokuja kwa mfalme, mfalme akamwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-gileadi vitani, au niache? Akasema, Kweeni, mkafanikiwe; nao watatiwa mikononi mwenu.
15. Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe, usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA?
16. Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji; BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.
17. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?
18. Mikaya akasema, Sikieni basi neno la BWANA; Nalimwona BWANA ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kuume na wa kushoto.
19. BWANA akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu mfalme wa Israeli, ili akwee Ramoth-gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.