1 Sam. 28:5-22 Swahili Union Version (SUV)

5. Basi alipowaona hao majeshi ya Wafilisti, huyo Sauli akaogopa, na moyo wake ukatetemeka sana.

6. Lakini Sauli alipouliza kwa BWANA, BWANA hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii.

7. Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori.

8. Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye na watu wawili pamoja naye, wakamfikilia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukanipandishie yeye nitakayemtaja kwako.

9. Yule mwanamke akamwambia, Angalia, unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili kuniua?

10. Naye Sauli akamwapia kwa BWANA, akasema, Aishivyo BWANA, haitakupata adhabu yo yote kwa jambo hili.

11. Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekupandishia? Naye akasema, Nipandishie Samweli.

12. Hata yule mwanamke alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli, akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli.

13. Mfalme akamwambia Usiogope; waona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu anatoka katika nchi.

14. Naye akamwuliza, Ni mfano wa nini? Akajibu, Ni mzee anazuka; naye amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe, akainama uso wake mpaka nchi, akasujudia.

15. Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Mbona umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu? Sauli akajibu, Mimi nimetaabika sana; kwa kuwa hao Wafilisti wananifanyia vita, naye Mungu ameniacha; hanijibu tena, wala kwa manabii, wala kwa ndoto; kwa hiyo nimekuita wewe, ili wewe unijulishe nifanyeje.

16. Samweli akasema, Kwa nini kuniuliza mimi, akiwa BWANA amekuacha, naye amekuwa adui yako?

17. Yeye BWANA amekutendea kama alivyosema kwa kinywa changu; BWANA amekurarulia ufalme mkononi mwako, na kumpa jirani yako, yaani, Daudi.

18. Kwa sababu wewe hukuitii sauti ya BWANA, wala hukumtimilizia hasira yake kali juu ya Amaleki; kwa sababu hii BWANA amekutendea hili leo.

19. Tena pamoja na wewe BWANA atawatia Israeli mikononi mwa Wafilisti; hata na kesho wewe na wanao mtakuwapo pamoja nami; tena BWANA atawatia jeshi la Israeli pia mikononi mwa Wafilisti.

20. Mara Sauli akaanguka chini kifulifuli, akaingiwa na hofu kuu kwa sababu ya maneno hayo ya Samweli, wala hakuwa na nguvu yo yote; kwa maana hakula chakula mchana kutwa, wala usiku kucha.

21. Ndipo yule mwanamke akamwendea Sauli, akamwona ya kuwa yeye ametaabika sana, akamwambia, Angalia, mjakazi wako ameisikiliza sauti yako, nami nimeutia uhai wangu mkononi mwangu, nami nimeyasikiliza maneno yako uliyoniambia.

22. Basi sasa, tafadhali, wewe uisikilize sauti ya mjakazi wako, nikakuandalie ngaa mkate kidogo; ukale, ili upate nguvu, utakapokwenda zako.

1 Sam. 28