1 Sam. 25:15-25 Swahili Union Version (SUV)

15. Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni;

16. watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo.

17. Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye.

18. Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda.

19. Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali.

20. Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kutelemka penye sitara ya mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta.

21. Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu cho chote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema.

22. Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi.

23. Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi.

24. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako.

25. Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma.

1 Sam. 25