15. Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni;
16. watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo.
17. Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye.
18. Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda.
19. Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali.
20. Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kutelemka penye sitara ya mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta.