24. Nao watu wa Israeli walisumbuka sana siku ile; lakini Sauli alikuwa amewaapisha watu, akisema, Na alaaniwe mtu awaye yote alaye chakula cho chote hata jioni, nipate kujilipiza kisasi juu ya adui zangu. Basi hakuna mtu miongoni mwa watu aliyeonja chakula.
25. Nao watu wote wakaingia mwituni; na humo mlikuwa na asali juu ya nchi.
26. Na hapo watu walipokwisha kuingia mwituni, tazama, hiyo asali ilikuwa ikidondoka; walakini hakuna mtu hata mmoja aliyetia mkono wake kinywani; kwa sababu hao watu walikuwa wakikiogopa kile kiapo.
27. Ila Yonathani hakusikia, hapo babaye alipowaagiza watu kwa kiapo; basi yeye akainyosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake, na kuichovya katika sega la asali, kisha akatia mkono wake kinywani; na macho yake yakatiwa nuru.
28. Ndipo mmojawapo wa watu akamjibu, akasema, Baba yako aliwaagiza watu sana kwa kiapo, akisema, Na alaaniwe mtu alaye chakula leo. Na hao watu walikuwa wamepungukiwa na nguvu.
29. Ndipo Yonathani akasema, Babangu ameifadhaisha nchi; tafadhali, angalia jinsi macho yangu yalivyotiwa nuru, kwa sababu nalionja asali hii kidogo.
30. Je! Si zaidi sana, kama watu wangalikula na kushiba leo katika nyara hizi za adui zao walizoziteka? Kwa maana haukuwa uuaji mkuu sasa katikati ya Wafilisti.
31. Nao wakawapiga watu miongoni mwa Wafilisti siku ile kutoka Mikmashi mpaka Ayaloni; na hao watu walikuwa wamepungukiwa sana na nguvu.
32. Basi watu wakazirukia zile nyara, wakatwaa kondoo, na ng’ombe, na ndama, na kuwachinja papo hapo juu ya nchi, nao wale watu walikuwa wakiwala pamoja na damu.
33. Ndipo wakamwambia Sauli, wakisema, Angalia, watu hao wanakosa juu ya BWANA, kwa jinsi wanavyokula pamoja na damu. Naye akasema, Ninyi mmefanya kwa hiana; vingirisheni kwangu leo jiwe kubwa.